Monday, 19 December 2011

MITIHANI SI HUKUMU!

Beti zifuatazo, nilitunga ili kuwapa moyo na kuwatakia kila lenye kheri na fanaka watahiniwa wote nchini wa darasa la nane walipokuwa wakiusubiri mtihani wa kitaifa wa K.C.P.E  Mwaka huu, 2011.

NASAHA ZA MITIHANI.
Ngu'zangu sabalkheri, nimerejea tungoni,
Naja kwenu na urari, ya nasaha niwapeni,
Ninalo wazo kitwani, naomba niwajuzeni,
Mitihani si janga, ni kigezo cha ubora.


Jambo hili si khiari, mitihani kufanyeni,
Lahitaji ujasiri, wanakwetu jikazeni,
Ufanisi kushamiri, bora uwe na makini,
Mitihani si maafa, ni kigezo cha ubingwa.


Yafaa uwe na ari, mja mwenye tumaini,
'Sianze kutahayari, ni bora ujiamini,
Hakikisha u tayari, ufikapo ukumbini,
Mitihani ni daraja, itakuvusha majini.


 Mitihani ni safari, huepuki maishani,
Watazame wahadhiri, mawakili na rubani,
Wote hao watakiri, walifanya mitihani,
Mitihani ndiyo dira, na ramani maishani.


Nawapeni tahadhari, 'sijipate taabani,
Maswali uyafasiri, usijitie mbioni,
Pupayo takuathiri, mitihani ukafeli,
Mitihani si adhabu, apewayo baradhuli.


Soma swali ubashiri, hoja zake mtahini,
Soma kila mistari, upitie kwa makini,
Hatiyo iwe nzuri, isiwe na walakini,
Mitihani ni mwongozo, kufikia ubingwani.


Usijiole mahiri, mitihani si utani,
Si vema kuwa jeuri, hamna maswali duni,
Mambo yote huwa shwari, kitulia akilini,
Mitihani si pigo, ni faraja kwa mweledi.


Watahini ni mahiri, watungapo mitihani,
Si rakhisi kubashiri, na mitego kubaini,
Yao nia si dhahiri, utadhani 'mahaini',
Mitihani si mzaha, sharti uwe na makini.


Kiamka alfajiri, piga dua kwa Manani,
Akuepushie shari, akili ziwe razini,
Atawatuza Khahari, hawaati abadani,
Mitihani si hukumu, ni hidaya za jamala .


Kaditama ninakiri, kwenda mbee sitamani,
Nawombeeni kheri, na fanaka maishani,
Atawapeni buheri, aloswifika Manani,
Mitihani ndiyo ngazi, kufikia kileleni.

Solomon ole Musere ,
Chuo kikuu cha Kenyatta
Nov 2, 2011

No comments:

Post a Comment