Friday, 16 December 2011

SI'BAGUE MLEMAVU

SI'BAGUE MLEMAVU

Nawaswabahi wendani,salamu zipokeeni,
Nawasihi sogeeni, na masikio nipeni,
Majibu kisha nipeni, nifikapo hatimani,
Sibague mlevavu, kwani mja mwenzako.

Mlemavu mwenye baa, ni yule mwenye kichaa,
Kwani awapo na njaa, hula hata kwenye jaa,
Huzua kubwa balaa, hatulii akakaa,
Si'bague mlemavu, kwani  mja mwenzako.

Aweza kuwa kipofu, subiri nikuarifu,
Akawa ni maarufu,kutunga nyimbo sanifu,
Ni mtunzi msarifu, lugha bora na faafu,
Si'bague mlemavu, kwani mja mwenzako.

  Kiwete hana miguu, japo hutenda makuu
Kazini 'tapanda juu, kushinda wenye miguu,
Watakuita mkuu, pasi na yako miguu,
Si'bague mlemavu, kwani mja mwenzako.

Ulemavu si kikwazo, kisiasa na michezo,
Mlemavu ana uwezo, kuongoza bila bezo,
Tamasha na tumbuizo,'takutia chachawizo,
Si'bague mlemavu, kwani mja mwenzako.

Japokuwa ni kiziwi,anao bora ujuzi,
Dosari katu hatiwi, taitwa hata mjuzi,
Daima habaguliwi,haina doa uziwi,
Si'bague mlemavu, kwani mja mwenzako.

Kuna wengi washairi, malenga walo mahiri,
Tungo zao mashuhuri, watunzi waso kiburi,
Zao tungo ni johari, zaonya na kushauri,
  Si'bague mlemavu, kwani mja mwenzako..

Hatima hapa natuwa, wangu wosia 'metowa,
Mlemavu kumbaguwa, mwenyewe wajiumbuwa,
Kikomoni ninatuwa, hili jamvi  nakunjuwa,
Si'bague mlemavu, kwani mja mwenzako.


Solomon ole Musere.
Chuo kikuu cha Kenyatta
       2011

No comments:

Post a Comment