Wednesday, 14 December 2011

MAKIWA WANAKENYATTA

MAKIWA WANAKENYATTA

Bisimillahi Rabuka,  illahi Mola Rahimu,
Mbelezo waja twafika,  twakulilia Rahimu;
Matozi yatudondoka,  twaomba uturehemu,
Makiwa wanakenyatta,  kumpoteza Ogeto.

Maafa yametuzuru,  mwenzetu yakatupoka,
Hakika yametudhuru,  nyoyoni twasononeka,
Tumeipoteza nuru,  ghafula imezimika,
Makiwa wanakenyatta,  kumpoteza Ogeto.

Mswiba umetuswibu,  ametuacha swahibu,
Tulimpenda ajabu,  halingani na dhahabu,
Hatuna katu majibu,  kwa kifo k'lichokuswibu,
Makiwa wanakenyatta,  kumpoteza Ogeto.

Nakumbuka hino siku,  'lipotuacha mpasi,
Saa mbili za usiku,  laili ya Jumamosi,
Huzuni ilitupiku,  ukatukumba mkosi,
Makiwa wanakenyatta,  kumpoteza Ogeto.

Ni pigo kwetu chuoni,  kumpoteza Ogeto,
'Metuachia huzuni,  na maisha ya majuto,
Tulikuenzi mwandani,  kipenzi chetu Ogeto,
Makiwa wanakenyatta,  kumpoteza Ogeto.

Rambi rambi nyingi sana,  ziwafikie nyumbani,
Farajaze Maulana,  kwa ndugu na majirani,
Inshallah tutamwona,  kipenzi chetu peponi,
Makiwa wanakenyatta,  kumpoteza Ogeto.

Nimefika kituoni,  machozi yanikupuka,
Poleni ndugu poleni,  ni matakwa ya Rabuka,
Alazwe pema peponi,  apate kusalimika,
Makiwa wanakenyatta,  kumpoteza Ogeto.

Solomon ole Musere
Chuo kikuu cha Kenyatta
Novemba 2011

No comments:

Post a Comment