Shairi hili nilitunga nikimwelekeza mwandani wangu,Samson Simpiri mwanagenzi wa maswala ya habari chuo cha ITI-Nairobi.
SUBIRA YAVUTA HERI .
Hujambo kaka Simpiri, sahibu mwanahabari?
Mepata wako urari, kujibu sina khiari,
Mwanetu ukae shwari, usome langu shairi ,
Mwandani stahimili, subira yavuta heri.
Mwanzo wa ngoma ni lele, msemo wa tangu kale,
Likaze sana fungule, faraja uje uole,
Muhibu katu silale, ‘dhamirayo ushikile,
Mwandani stahimili, subira yavuta heri.
‘Kitembea mitaani, Nairobi hapo mjini,
Uwe makini mwandani, sije ‘ingia dhikini ,
Ewe jimbi la kondeni, huyajui ya jijini,
Mwandani stahimili, subira yavuta heri.
Moja siku itafika, Simpiri utatajika,
Zifazo ‘taenezeka, kama moto kwenye chaka,
Wakuite msifika, moyoni nitaridhika,
Mwandani stahimili, subira yavuta heri.
Nanena kweli muhibu, sipendi kukughilibu,
Dunia ina taabu,na wingi wa masaibu,
Uchunge ustaarabu, mikosi isikuswibu,
Mwandani stahimili, subira yavuta heri.
Kumbuka huko Nkareta, wazee tulowaata,
Mabegi tukapakata, baraste tukafuata,
Vyuoni tukajipata, weledi kuutafuta,
Mwandani stahimili, subira yavuta heri.
Nakuamini mwandani, ya kuwa u razini,
Mzawa wa kijijini, mtunzi mwenye imani,
Hauna maji kitwani, huna katu walakini,
Mwandani stahimili, subira yavuta heri.
Sahibu 'jikaze sana, uwe mja wa dhamana,
Usiwe mwenye fitina, wala mwingi wa khiana,
Na mtukufu Rabana, akuepushe laana,
Mwandani stahimili, subira yavuta heri.
Hapa ndipo ninatuwa, Musere ninapumuwa,
Wosia n'shautowa, na mzigo kuutuwa,
Rabuka nampa duwa, kanipa hii satuwa,
Mwandani stahimili, subira yavuta heri.
SOLOMON OLE MUSERE'
'Malenga mwitu'
CHUO KIKUU CHA KENYATTA
NOV, 2011
No comments:
Post a Comment