Monday, 19 December 2011

PUNGUZENI VIPODOZI

Hakika inavunja moyo kuona jinsi wengi wetu tunavyopenda kutumia vipodozi, kiasi cha kuifuja ngozi, uzuri na haiba ya kipekee tuliojaliwa na Muumba! Naam, si vibaya kujipodoa, lakini ukizidisha basi unajipunguzia uzuri, mvuto na  isitoshe,kuivuruga haiba ya wajihi na hadhi  yako pia!
TUTHAMINI "UREMBO WA KIWETU!"

PUNGUZENI VIPODOZI.
Kuna tendo lanighasi, nilionalo ni hasi,
Linaibua utesi, na hisia za uasi,
Ninalipinga kwa kasi, natangaza wasiwasi,
Punguzeni vipodozi, vinapunguza  haiba.

Ninashindwa kutambua, kwanini mwajiumbua,
Hili swala lazuzua, natamani kung'amua,
Nawaza nikiwazua, kamwe sijalitambua,
Punguzeni vipodozi, vinapunguza haiba.

Silika ino'chukiza, kulla jambo kuigiza,
Tuliumbwa kupendeza, kwanini twajichakaza?
Yafaa kumtukuza, Muumba alo Muweza,
Punguzeni vipodozi, vinapunguza haiba.

Ewe binti mwafrika, tizama 'livyoumbika,
Urembo wa malaika, kokote watamanika,
Weusi ulioshika, hakika unapendeka,
Punguzeni vipodozi, vinapunguza haiba.

'Mepewa ngozi laini, nyororo iso kifani,
Ukaona haifani, alivyoumba Manani,
Ukajifuja kwa kani, vipodozi kusheheni,
Punguzeni vipodozi, vinapunguza haiba.

Vipuli masikioni, na mikufu ya shingoni,
Mwajitoga sikioni, utungu kujitieni,
Wekundu wa mdomoni, ni upi wake thamani ?
Punguzeni vipodozi, vinapunguza haiba.

Kuchazo mwapaka hina, mkidhani mtafana,
Nyengine ni ndefu sana, zatisha ukiziona,
Umuonapo kimwana, mhanga amefanana!
Punguzeni vipodozi, vinapunguza haiba.

Rangi hino maozini,thamani katu sioni,
'Kivaa vingi vipini, uzuri kamwe hunani,
Ndonya 'kitia puani, watangaza jambo gani?
Punguzeni vipodozi, vinapunguza haiba.

Tisa beti timilifu, hatima imesadifu,
Musere nakuarifu, ufate nyendo 'faafu,
Tuzidi kujinadhifu, apendavyo Mtukufu,
Punguzeni vipodozi, vinapunguza haiba.

SOLOMON OLE MUSERE,
'Malenga mwitu'
CHUO KIKUU CHA KENYATTA.

No comments:

Post a Comment