WARIDI WANGU
Kamwe sifanyi ajizi, kalamu nakumbatiya
Ya muhimu maongezi, sitaki kukiakiya,
Umenikoleza penzi, nazunguka kama piya,
Ua langu la waridi, ninakuenzi kimwana.
Ewe ni jizi mahiri, uloiba cha thamani,
Meinyakuwa suduri, na mawazo matekani,
Bila soni nakariri, nimebaki kifungoni,
Ua langu la waridi, ninakuenzi kimwana.
Moyoni sina terema, kiwa mbali na waridi,
Malaika husimama, nikumbukapo miadi,
Malaji hayawi mema , upweke kweli hasidi,
Ua langu la waridi, ninakuenzi kimwana.
Popote nikitembeya , sitakuacha mahabubu,
Pichayo mejibebeya, mapuzi yasinisibu,
Moyini mekufichiya, uwe wangu taabibu,
Ua langu la waridi, ninakuenzi kimwana.
Japo ni mengi masafa, kukuwazia sichoki,
N'japokumbwa na maafa , moyoni mwangu hutoki,
Ninaposoma arafa, moyoni ninaafiki,
Ua langu la waridi, ninakuenzi kimwana.
Mtoto umeumbika, Rabana halaumiki,
Kisura u malaika, mannenoyo kama uki,
Hurulaini msifika, katu sina unafiki,
Ua langu la waridi, ninakuenzi kimwana.
Moyoni nitakubana, kwa aushi na mauti,
Uwe wangu wa dhamana , hata kama sina suti,
Daima tutafaaana, kwa mapenzi madhubuti,
Ua langu la waridi, ninakuenzi kimwana.
Kwa kufunga ukurasa, unalo kubwa wajibu,
Ujibari na siasa, ya nduli wasoaibu,
Kidege ninakuasa, wasome kama kitabu,
Ua langu la waridi, ninakuenzi kimwana.
Kuhitimisha shairi, nina dua kwa Khahari,
Atuepushe kiburi, na lolote lenye shari,
Lisigeuke shubiri, mapenzi na yashamiri,
Ua langu la waridi, ninakuenzi kimwana.
Hadi hapo ninatuwa, kwenda mbee nimeasi,
Maneno chukuwa, yasuke kama msusi,
Langu dau nalishuwa, memaliza ujasusi,
Ua langu la waridi, ninakuenzi kimwana.
SOLOMON OLE MUSERE,
CHUO KIKUU CHA KENYATTA.
No comments:
Post a Comment