KILIO CHA MKIMBIZI
Bismillahi mhariri, nakuletea shairi,
Yaweke haya dhahiri, kilio kisiwe siri,
Wakimbizi tuna shari, maisha kwetu shubiri,
Wakimbizi wana haki, acheni zenu hujuma.
Si shibe seuze vazi, kila kutwa ni matozi,
Mkimbizi hana kazi, hawi hata kijakazi,
Nawaomba kwa uwazi, kujibari ubaguzi,
Wakimbizi wana haki, acheni zenu hujuma.
Viongozi nambieni, msikane asilani,
Macho yenu hayaoni, kuwa sie tu dhikini?
Mwatuona hayawani, viumbe wenye punguani,
Wakimbizi wana haki, acheni zenu hujuma.
Mkimbizi ana haki, nasema kwa uhakiki,
Makao si handaki, na malazi bila dhiki,
Si vema kuwadhihaki, wakenya kindakindaki,
Wakimbizi wana haki, acheni zenu hujuma.
Bendera tulizowapa, mkaanza kujitapa,
Ulaya hata Uropa, mwapaa hata kwa chopa,
Wakimbizi tunaapa,zetu kura kutowapa,
Wakimbizi wana haki, acheni zenu hujuma.
Inshallah hapo mwakani, zijapo hizo kampeni,
Pasi na haya nyusoni, mtarudi mitaani,
Ujanja huo wa nyani, utaishia jangwani,
Wakimbizi wana haki, acheni zenu hujuma.
Kedi tama wa tamati, narudi zangu kambini,
Ujumbe huu wa dhati, ufike hata bungeni,
Zetu dhiki ainati, hayaishi abadani,
Wakimbizi wana haki, acheni zenu hujuma.
Solomon ole Musere
Chuo kikuu cha Kenyatta
2011
No comments:
Post a Comment