ULIYATAKA MWENYEWE,
Mrembo nakuswabahi,natumai u buheri,
Fursa hino naiwahi, kukuasa kishairi,
Nanena yalo sahihi,nikwambile pasi siri,
Uliyataka mwenyewe, na sasa kilio chani?
Kidosho nilikupenda,posa nikakuletile,
Nawe juu ukapanda,kuwa mie mchochole,
Nenda basi mwanakwenda, Musere nikakwambile
Uliyataka mwenyewe, na sasa kilio chani?
Bwanyanye kakughilibu,ukawa windo rakhisi,
Ukalikumbatia dubu, kwa tamaa ya ukwasi,
Kirinda pasi aibu, kikakutoka kwa kasi,
Uliyataka mwenyewe, na sasa kilio chani?
Mhuni ukampa fursa, lako tunda kulimega,
Mkazamia anasa, mahaba yaliponoga,
Kila siku kawa misa, kokote mkijibwaga,
Uliyataka mwenyewe, na sasa kilio chani?
Dunia hutoiweza, nilikupa mausiya,
Matusi 'kanilekeza, kisema nakuchongeya,
Ukajigeuza pweza, makaa kujipaliya,
Uliyataka mwenyewe, na sasa kilio chani?
Hakika niliumiya,kimwana ulipozama,
Mengi nilokutendeya, ukaleta uhasama,
Kabidi kunyamaziya,kwa soni nikiinama,
Uliyataka mwenyewe, na sasa kilio chani?
Haikupita miezi, akakuponyoka Keni,
Likavuruga penzi, kitumbua mchangani,
Ukaachwa na matozi, na ndwele humo mwilini
Uliyataka mwenyewe, na sasa kilio chani?
Katu huoni fedheha, eti wajileta kwangu?
'Sitaraji msamaha, hilo muuze Mungu,
Ulotenda ni karaha,yalinitia utungu,
Uliyataka mwenyewe, na sasa kilio chani?
Kikomo ninapotia, kidosho ushasikia,
Katu sitochelea,ukweli kukuambia,
Hilo kero fikiria, ndo ujumbe nakuatia,
Uliyataka mwenyewe, na sasa kilio chani?
SOLOMON MUSERE, FEB 2012.
CHUO KIKUU CHA KENYATTA
No comments:
Post a Comment