Beti zifuatazo, nilitunga ili kuwapa moyo na kuwatakia kila lenye kheri na fanaka watahiniwa wote nchini wa darasa la nane walipokuwa wakiusubiri mtihani wa kitaifa wa K.C.P.E Mwaka huu, 2011.
NASAHA ZA MITIHANI.
Ngu'zangu sabalkheri, nimerejea tungoni,
Naja kwenu na urari, ya nasaha niwapeni,
Ninalo wazo kitwani, naomba niwajuzeni,
Mitihani si janga, ni kigezo cha ubora.
Jambo hili si khiari, mitihani kufanyeni,
Lahitaji ujasiri, wanakwetu jikazeni,
Ufanisi kushamiri, bora uwe na makini,
Mitihani si maafa, ni kigezo cha ubingwa.
Yafaa uwe na ari, mja mwenye tumaini,
'Sianze kutahayari, ni bora ujiamini,
Hakikisha u tayari, ufikapo ukumbini,
Mitihani ni daraja, itakuvusha majini.
Mitihani ni safari, huepuki maishani,
Watazame wahadhiri, mawakili na rubani,
Wote hao watakiri, walifanya mitihani,
Mitihani ndiyo dira, na ramani maishani.
Nawapeni tahadhari, 'sijipate taabani,
Maswali uyafasiri, usijitie mbioni,
Pupayo takuathiri, mitihani ukafeli,
Mitihani si adhabu, apewayo baradhuli.
Soma swali ubashiri, hoja zake mtahini,
Soma kila mistari, upitie kwa makini,
Hatiyo iwe nzuri, isiwe na walakini,
Mitihani ni mwongozo, kufikia ubingwani.
Usijiole mahiri, mitihani si utani,
Si vema kuwa jeuri, hamna maswali duni,
Mambo yote huwa shwari, kitulia akilini,
Mitihani si pigo, ni faraja kwa mweledi.
Watahini ni mahiri, watungapo mitihani,
Si rakhisi kubashiri, na mitego kubaini,
Yao nia si dhahiri, utadhani 'mahaini',
Mitihani si mzaha, sharti uwe na makini.
Kiamka alfajiri, piga dua kwa Manani,
Akuepushie shari, akili ziwe razini,
Atawatuza Khahari, hawaati abadani,
Mitihani si hukumu, ni hidaya za jamala .
Kaditama ninakiri, kwenda mbee sitamani,
Nawombeeni kheri, na fanaka maishani,
Atawapeni buheri, aloswifika Manani,
Mitihani ndiyo ngazi, kufikia kileleni.
Solomon ole Musere ,
Chuo kikuu cha Kenyatta
Nov 2, 2011
Monday, 19 December 2011
PUNGUZENI VIPODOZI
Hakika inavunja moyo kuona jinsi wengi wetu tunavyopenda kutumia vipodozi, kiasi cha kuifuja ngozi, uzuri na haiba ya kipekee tuliojaliwa na Muumba! Naam, si vibaya kujipodoa, lakini ukizidisha basi unajipunguzia uzuri, mvuto na isitoshe,kuivuruga haiba ya wajihi na hadhi yako pia!
TUTHAMINI "UREMBO WA KIWETU!"
PUNGUZENI VIPODOZI.
Kuna tendo lanighasi, nilionalo ni hasi,
Linaibua utesi, na hisia za uasi,
Ninalipinga kwa kasi, natangaza wasiwasi,
Punguzeni vipodozi, vinapunguza haiba.
Ninashindwa kutambua, kwanini mwajiumbua,
Hili swala lazuzua, natamani kung'amua,
Nawaza nikiwazua, kamwe sijalitambua,
Punguzeni vipodozi, vinapunguza haiba.
Silika ino'chukiza, kulla jambo kuigiza,
Tuliumbwa kupendeza, kwanini twajichakaza?
Yafaa kumtukuza, Muumba alo Muweza,
Punguzeni vipodozi, vinapunguza haiba.
Ewe binti mwafrika, tizama 'livyoumbika,
Urembo wa malaika, kokote watamanika,
Weusi ulioshika, hakika unapendeka,
Punguzeni vipodozi, vinapunguza haiba.
'Mepewa ngozi laini, nyororo iso kifani,
Ukaona haifani, alivyoumba Manani,
Ukajifuja kwa kani, vipodozi kusheheni,
Punguzeni vipodozi, vinapunguza haiba.
Vipuli masikioni, na mikufu ya shingoni,
Mwajitoga sikioni, utungu kujitieni,
Wekundu wa mdomoni, ni upi wake thamani ?
Punguzeni vipodozi, vinapunguza haiba.
Kuchazo mwapaka hina, mkidhani mtafana,
Nyengine ni ndefu sana, zatisha ukiziona,
Umuonapo kimwana, mhanga amefanana!
Punguzeni vipodozi, vinapunguza haiba.
Rangi hino maozini,thamani katu sioni,
'Kivaa vingi vipini, uzuri kamwe hunani,
Ndonya 'kitia puani, watangaza jambo gani?
Punguzeni vipodozi, vinapunguza haiba.
Tisa beti timilifu, hatima imesadifu,
Musere nakuarifu, ufate nyendo 'faafu,
Tuzidi kujinadhifu, apendavyo Mtukufu,
Punguzeni vipodozi, vinapunguza haiba.
SOLOMON OLE MUSERE,
'Malenga mwitu'
CHUO KIKUU CHA KENYATTA.
TUTHAMINI "UREMBO WA KIWETU!"
PUNGUZENI VIPODOZI.
Kuna tendo lanighasi, nilionalo ni hasi,
Linaibua utesi, na hisia za uasi,
Ninalipinga kwa kasi, natangaza wasiwasi,
Punguzeni vipodozi, vinapunguza haiba.
Ninashindwa kutambua, kwanini mwajiumbua,
Hili swala lazuzua, natamani kung'amua,
Nawaza nikiwazua, kamwe sijalitambua,
Punguzeni vipodozi, vinapunguza haiba.
Silika ino'chukiza, kulla jambo kuigiza,
Tuliumbwa kupendeza, kwanini twajichakaza?
Yafaa kumtukuza, Muumba alo Muweza,
Punguzeni vipodozi, vinapunguza haiba.
Ewe binti mwafrika, tizama 'livyoumbika,
Urembo wa malaika, kokote watamanika,
Weusi ulioshika, hakika unapendeka,
Punguzeni vipodozi, vinapunguza haiba.
'Mepewa ngozi laini, nyororo iso kifani,
Ukaona haifani, alivyoumba Manani,
Ukajifuja kwa kani, vipodozi kusheheni,
Punguzeni vipodozi, vinapunguza haiba.
Vipuli masikioni, na mikufu ya shingoni,
Mwajitoga sikioni, utungu kujitieni,
Wekundu wa mdomoni, ni upi wake thamani ?
Punguzeni vipodozi, vinapunguza haiba.
Kuchazo mwapaka hina, mkidhani mtafana,
Nyengine ni ndefu sana, zatisha ukiziona,
Umuonapo kimwana, mhanga amefanana!
Punguzeni vipodozi, vinapunguza haiba.
Rangi hino maozini,thamani katu sioni,
'Kivaa vingi vipini, uzuri kamwe hunani,
Ndonya 'kitia puani, watangaza jambo gani?
Punguzeni vipodozi, vinapunguza haiba.
Tisa beti timilifu, hatima imesadifu,
Musere nakuarifu, ufate nyendo 'faafu,
Tuzidi kujinadhifu, apendavyo Mtukufu,
Punguzeni vipodozi, vinapunguza haiba.
SOLOMON OLE MUSERE,
'Malenga mwitu'
CHUO KIKUU CHA KENYATTA.
Friday, 16 December 2011
SI'BAGUE MLEMAVU
SI'BAGUE MLEMAVU
Nawaswabahi wendani,salamu zipokeeni,Nawasihi sogeeni, na masikio nipeni,
Majibu kisha nipeni, nifikapo hatimani,
Sibague mlevavu, kwani mja mwenzako.
Mlemavu mwenye baa, ni yule mwenye kichaa,
Kwani awapo na njaa, hula hata kwenye jaa,
Huzua kubwa balaa, hatulii akakaa,
Si'bague mlemavu, kwani mja mwenzako.
Aweza kuwa kipofu, subiri nikuarifu,
Akawa ni maarufu,kutunga nyimbo sanifu,
Ni mtunzi msarifu, lugha bora na faafu,
Si'bague mlemavu, kwani mja mwenzako.
Kiwete hana miguu, japo hutenda makuu
Kazini 'tapanda juu, kushinda wenye miguu,
Watakuita mkuu, pasi na yako miguu,
Si'bague mlemavu, kwani mja mwenzako.
Ulemavu si kikwazo, kisiasa na michezo,
Mlemavu ana uwezo, kuongoza bila bezo,
Tamasha na tumbuizo,'takutia chachawizo,
Si'bague mlemavu, kwani mja mwenzako.
Japokuwa ni kiziwi,anao bora ujuzi,
Dosari katu hatiwi, taitwa hata mjuzi,
Daima habaguliwi,haina doa uziwi,
Si'bague mlemavu, kwani mja mwenzako.
Kuna wengi washairi, malenga walo mahiri,
Tungo zao mashuhuri, watunzi waso kiburi,
Zao tungo ni johari, zaonya na kushauri,
Si'bague mlemavu, kwani mja mwenzako..
Hatima hapa natuwa, wangu wosia 'metowa,
Mlemavu kumbaguwa, mwenyewe wajiumbuwa,
Kikomoni ninatuwa, hili jamvi nakunjuwa,
Si'bague mlemavu, kwani mja mwenzako.
Solomon ole Musere.
Chuo kikuu cha Kenyatta
2011
UA LANGU.
WARIDI WANGU
Kamwe sifanyi ajizi, kalamu nakumbatiya
Ya muhimu maongezi, sitaki kukiakiya,
Umenikoleza penzi, nazunguka kama piya,
Ua langu la waridi, ninakuenzi kimwana.
Ewe ni jizi mahiri, uloiba cha thamani,
Meinyakuwa suduri, na mawazo matekani,
Bila soni nakariri, nimebaki kifungoni,
Ua langu la waridi, ninakuenzi kimwana.
Moyoni sina terema, kiwa mbali na waridi,
Malaika husimama, nikumbukapo miadi,
Malaji hayawi mema , upweke kweli hasidi,
Ua langu la waridi, ninakuenzi kimwana.
Popote nikitembeya , sitakuacha mahabubu,
Pichayo mejibebeya, mapuzi yasinisibu,
Moyini mekufichiya, uwe wangu taabibu,
Ua langu la waridi, ninakuenzi kimwana.
Japo ni mengi masafa, kukuwazia sichoki,
N'japokumbwa na maafa , moyoni mwangu hutoki,
Ninaposoma arafa, moyoni ninaafiki,
Ua langu la waridi, ninakuenzi kimwana.
Mtoto umeumbika, Rabana halaumiki,
Kisura u malaika, mannenoyo kama uki,
Hurulaini msifika, katu sina unafiki,
Ua langu la waridi, ninakuenzi kimwana.
Moyoni nitakubana, kwa aushi na mauti,
Uwe wangu wa dhamana , hata kama sina suti,
Daima tutafaaana, kwa mapenzi madhubuti,
Ua langu la waridi, ninakuenzi kimwana.
Kwa kufunga ukurasa, unalo kubwa wajibu,
Ujibari na siasa, ya nduli wasoaibu,
Kidege ninakuasa, wasome kama kitabu,
Ua langu la waridi, ninakuenzi kimwana.
Kuhitimisha shairi, nina dua kwa Khahari,
Atuepushe kiburi, na lolote lenye shari,
Lisigeuke shubiri, mapenzi na yashamiri,
Ua langu la waridi, ninakuenzi kimwana.
Hadi hapo ninatuwa, kwenda mbee nimeasi,
Maneno chukuwa, yasuke kama msusi,
Langu dau nalishuwa, memaliza ujasusi,
Ua langu la waridi, ninakuenzi kimwana.
SOLOMON OLE MUSERE,
CHUO KIKUU CHA KENYATTA.
Kamwe sifanyi ajizi, kalamu nakumbatiya
Ya muhimu maongezi, sitaki kukiakiya,
Umenikoleza penzi, nazunguka kama piya,
Ua langu la waridi, ninakuenzi kimwana.
Ewe ni jizi mahiri, uloiba cha thamani,
Meinyakuwa suduri, na mawazo matekani,
Bila soni nakariri, nimebaki kifungoni,
Ua langu la waridi, ninakuenzi kimwana.
Moyoni sina terema, kiwa mbali na waridi,
Malaika husimama, nikumbukapo miadi,
Malaji hayawi mema , upweke kweli hasidi,
Ua langu la waridi, ninakuenzi kimwana.
Popote nikitembeya , sitakuacha mahabubu,
Pichayo mejibebeya, mapuzi yasinisibu,
Moyini mekufichiya, uwe wangu taabibu,
Ua langu la waridi, ninakuenzi kimwana.
Japo ni mengi masafa, kukuwazia sichoki,
N'japokumbwa na maafa , moyoni mwangu hutoki,
Ninaposoma arafa, moyoni ninaafiki,
Ua langu la waridi, ninakuenzi kimwana.
Mtoto umeumbika, Rabana halaumiki,
Kisura u malaika, mannenoyo kama uki,
Hurulaini msifika, katu sina unafiki,
Ua langu la waridi, ninakuenzi kimwana.
Moyoni nitakubana, kwa aushi na mauti,
Uwe wangu wa dhamana , hata kama sina suti,
Daima tutafaaana, kwa mapenzi madhubuti,
Ua langu la waridi, ninakuenzi kimwana.
Kwa kufunga ukurasa, unalo kubwa wajibu,
Ujibari na siasa, ya nduli wasoaibu,
Kidege ninakuasa, wasome kama kitabu,
Ua langu la waridi, ninakuenzi kimwana.
Kuhitimisha shairi, nina dua kwa Khahari,
Atuepushe kiburi, na lolote lenye shari,
Lisigeuke shubiri, mapenzi na yashamiri,
Ua langu la waridi, ninakuenzi kimwana.
Hadi hapo ninatuwa, kwenda mbee nimeasi,
Maneno chukuwa, yasuke kama msusi,
Langu dau nalishuwa, memaliza ujasusi,
Ua langu la waridi, ninakuenzi kimwana.
SOLOMON OLE MUSERE,
CHUO KIKUU CHA KENYATTA.
SUBIRA.
Shairi hili nilitunga nikimwelekeza mwandani wangu,Samson Simpiri mwanagenzi wa maswala ya habari chuo cha ITI-Nairobi.
SUBIRA YAVUTA HERI .
Hujambo kaka Simpiri, sahibu mwanahabari?
Mepata wako urari, kujibu sina khiari,
Mwanetu ukae shwari, usome langu shairi ,
Mwandani stahimili, subira yavuta heri.
Mwanzo wa ngoma ni lele, msemo wa tangu kale,
Likaze sana fungule, faraja uje uole,
Muhibu katu silale, ‘dhamirayo ushikile,
Mwandani stahimili, subira yavuta heri.
‘Kitembea mitaani, Nairobi hapo mjini,
Uwe makini mwandani, sije ‘ingia dhikini ,
Ewe jimbi la kondeni, huyajui ya jijini,
Mwandani stahimili, subira yavuta heri.
Moja siku itafika, Simpiri utatajika,
Zifazo ‘taenezeka, kama moto kwenye chaka,
Wakuite msifika, moyoni nitaridhika,
Mwandani stahimili, subira yavuta heri.
Nanena kweli muhibu, sipendi kukughilibu,
Dunia ina taabu,na wingi wa masaibu,
Uchunge ustaarabu, mikosi isikuswibu,
Mwandani stahimili, subira yavuta heri.
Kumbuka huko Nkareta, wazee tulowaata,
Mabegi tukapakata, baraste tukafuata,
Vyuoni tukajipata, weledi kuutafuta,
Mwandani stahimili, subira yavuta heri.
Nakuamini mwandani, ya kuwa u razini,
Mzawa wa kijijini, mtunzi mwenye imani,
Hauna maji kitwani, huna katu walakini,
Mwandani stahimili, subira yavuta heri.
Sahibu 'jikaze sana, uwe mja wa dhamana,
Usiwe mwenye fitina, wala mwingi wa khiana,
Na mtukufu Rabana, akuepushe laana,
Mwandani stahimili, subira yavuta heri.
Hapa ndipo ninatuwa, Musere ninapumuwa,
Wosia n'shautowa, na mzigo kuutuwa,
Rabuka nampa duwa, kanipa hii satuwa,
Mwandani stahimili, subira yavuta heri.
SOLOMON OLE MUSERE'
'Malenga mwitu'
CHUO KIKUU CHA KENYATTA
NOV, 2011
SUBIRA YAVUTA HERI .
Hujambo kaka Simpiri, sahibu mwanahabari?
Mepata wako urari, kujibu sina khiari,
Mwanetu ukae shwari, usome langu shairi ,
Mwandani stahimili, subira yavuta heri.
Mwanzo wa ngoma ni lele, msemo wa tangu kale,
Likaze sana fungule, faraja uje uole,
Muhibu katu silale, ‘dhamirayo ushikile,
Mwandani stahimili, subira yavuta heri.
‘Kitembea mitaani, Nairobi hapo mjini,
Uwe makini mwandani, sije ‘ingia dhikini ,
Ewe jimbi la kondeni, huyajui ya jijini,
Mwandani stahimili, subira yavuta heri.
Moja siku itafika, Simpiri utatajika,
Zifazo ‘taenezeka, kama moto kwenye chaka,
Wakuite msifika, moyoni nitaridhika,
Mwandani stahimili, subira yavuta heri.
Nanena kweli muhibu, sipendi kukughilibu,
Dunia ina taabu,na wingi wa masaibu,
Uchunge ustaarabu, mikosi isikuswibu,
Mwandani stahimili, subira yavuta heri.
Kumbuka huko Nkareta, wazee tulowaata,
Mabegi tukapakata, baraste tukafuata,
Vyuoni tukajipata, weledi kuutafuta,
Mwandani stahimili, subira yavuta heri.
Nakuamini mwandani, ya kuwa u razini,
Mzawa wa kijijini, mtunzi mwenye imani,
Hauna maji kitwani, huna katu walakini,
Mwandani stahimili, subira yavuta heri.
Sahibu 'jikaze sana, uwe mja wa dhamana,
Usiwe mwenye fitina, wala mwingi wa khiana,
Na mtukufu Rabana, akuepushe laana,
Mwandani stahimili, subira yavuta heri.
Hapa ndipo ninatuwa, Musere ninapumuwa,
Wosia n'shautowa, na mzigo kuutuwa,
Rabuka nampa duwa, kanipa hii satuwa,
Mwandani stahimili, subira yavuta heri.
SOLOMON OLE MUSERE'
'Malenga mwitu'
CHUO KIKUU CHA KENYATTA
NOV, 2011
Thursday, 15 December 2011
UTANGULIZI
Naam, mie ni ghulamu anayeibuka katika sanaa hii ya utunzi wa mashairi.Bado sijawa malenga hasa bali ningali najaribisha tu katika harakati za kujifunza na kujizoesha uga wenyewe.Sijafuzu bado katika ngoma hii lakini dua yangu ni kuwa, siku moja nitakuwa sogora wa kupigiwa mifano kote katika fani ya utunzi.
Azma yangu ya utunzi ilichipuka nilipokuwa katika kidato cha pili, nikaanza kushiriki mashindano ya utunzi na kukariri mashairi kwenye tamasha ya muziki ya shule za upili.Ingawa sikufika mbali, niliwakisha shule yetu katika mashindano ya wilaya na mkoa wa Nairobi na hii ilinipa ari na motisha ya kuendelea kupiga mbizi katika bahari hii yenye kina kirefu.Sasa hivi, mimi ni mwanagenzi wa maswala ya elimu katika chuo kikuu cha Kenyatta.
Waama, naienzi, naithamini na kuihusudu lugha hii tukufu ya Kiswahili.Kwa yeyote atayepata fursa na satua ya kuyasoma mashairi yangu, nitakuwa na terema sufufu na maridhawa ukichukua nafasi yako kunishauri,kunipongeza, kunielekeza na kunipa changamoto.Kumbuka kinga na kinga ndipo moto uwakapo na daima geza geza mji huwa! TUSAIDIANETUZIDI KUIENZI NA KUIHUSUDU LUGHA HII, KOTE KOTE.
SHUKRANI.
SOLOMON OLE MUSERE.
CHUO KIKUU CHA KENYATTA.
Wednesday, 14 December 2011
MKIMBIZI ANA HAKI
KILIO CHA MKIMBIZI
Bismillahi mhariri, nakuletea shairi,
Yaweke haya dhahiri, kilio kisiwe siri,
Wakimbizi tuna shari, maisha kwetu shubiri,
Wakimbizi wana haki, acheni zenu hujuma.
Si shibe seuze vazi, kila kutwa ni matozi,
Mkimbizi hana kazi, hawi hata kijakazi,
Nawaomba kwa uwazi, kujibari ubaguzi,
Wakimbizi wana haki, acheni zenu hujuma.
Viongozi nambieni, msikane asilani,
Macho yenu hayaoni, kuwa sie tu dhikini?
Mwatuona hayawani, viumbe wenye punguani,
Wakimbizi wana haki, acheni zenu hujuma.
Mkimbizi ana haki, nasema kwa uhakiki,
Makao si handaki, na malazi bila dhiki,
Si vema kuwadhihaki, wakenya kindakindaki,
Wakimbizi wana haki, acheni zenu hujuma.
Bendera tulizowapa, mkaanza kujitapa,
Ulaya hata Uropa, mwapaa hata kwa chopa,
Wakimbizi tunaapa,zetu kura kutowapa,
Wakimbizi wana haki, acheni zenu hujuma.
Inshallah hapo mwakani, zijapo hizo kampeni,
Pasi na haya nyusoni, mtarudi mitaani,
Ujanja huo wa nyani, utaishia jangwani,
Wakimbizi wana haki, acheni zenu hujuma.
Kedi tama wa tamati, narudi zangu kambini,
Ujumbe huu wa dhati, ufike hata bungeni,
Zetu dhiki ainati, hayaishi abadani,
Wakimbizi wana haki, acheni zenu hujuma.
Solomon ole Musere
Chuo kikuu cha Kenyatta
2011
Bismillahi mhariri, nakuletea shairi,
Yaweke haya dhahiri, kilio kisiwe siri,
Wakimbizi tuna shari, maisha kwetu shubiri,
Wakimbizi wana haki, acheni zenu hujuma.
Si shibe seuze vazi, kila kutwa ni matozi,
Mkimbizi hana kazi, hawi hata kijakazi,
Nawaomba kwa uwazi, kujibari ubaguzi,
Wakimbizi wana haki, acheni zenu hujuma.
Viongozi nambieni, msikane asilani,
Macho yenu hayaoni, kuwa sie tu dhikini?
Mwatuona hayawani, viumbe wenye punguani,
Wakimbizi wana haki, acheni zenu hujuma.
Mkimbizi ana haki, nasema kwa uhakiki,
Makao si handaki, na malazi bila dhiki,
Si vema kuwadhihaki, wakenya kindakindaki,
Wakimbizi wana haki, acheni zenu hujuma.
Bendera tulizowapa, mkaanza kujitapa,
Ulaya hata Uropa, mwapaa hata kwa chopa,
Wakimbizi tunaapa,zetu kura kutowapa,
Wakimbizi wana haki, acheni zenu hujuma.
Inshallah hapo mwakani, zijapo hizo kampeni,
Pasi na haya nyusoni, mtarudi mitaani,
Ujanja huo wa nyani, utaishia jangwani,
Wakimbizi wana haki, acheni zenu hujuma.
Kedi tama wa tamati, narudi zangu kambini,
Ujumbe huu wa dhati, ufike hata bungeni,
Zetu dhiki ainati, hayaishi abadani,
Wakimbizi wana haki, acheni zenu hujuma.
Solomon ole Musere
Chuo kikuu cha Kenyatta
2011
MARINDA UFUPISHAPO
MARINDA UFUPISHAPO,
Naketi na kutuliya, na tungo nawatungiya,
Nanena ya mausiya, mabinti waje sikiya,
Nakuomba karibiya, usije ukasusiya,
Marinda ufupishapo, hahiyo wajishushia.
Mavazi yanayoruka, sitamani kujivika,
Mapaja kubainika, sidhani utapendeka,
Maungo yakifichuka, huwezi kutamanika,
Marinda ufupishapo, hadhiyo wajishushia,
.
Marinda yanayobana, tangu lini yakafana?
Akivalia kimwana, mwenyewe ajitukana,
Wazee wakiwaona, mwajitakia laana,
Marinda ufupishapo, hahiyo wajishushia .
Mavazi yasosetiri, hakika yana ghururi,
Minofu ikithihiri, mwadhani ni umahiri?
Maungo kiwa dhahiri, laana yawasubiri,
Marinda ufupishapo, hadhiyo wajishushia.
Kivaa minisketi, tashindwa hata kuketi,
Watuonyesha magoti, mapaja kama majiti,
Maguu lau makuti, haina haiba eti,
Marinda ufupishapo, hadhiyo wajishushia.
Vazi ni fupi jamani, mwalipasua mbeleni?
Hamna haya usoni, hata kule kanisani,
Mwajivalia kihuni, hata m'wapo nyumbani,
Marinda ufushapo, hadhiyo wajishushia.
Hadi hapo mabenati, nimefikia tamati,
Mawaidha siyaati, ni ombi si sharuti,
Nawashukuru kwa dhati, kwa kunipeni wakati,
Marinda ufupisapo, hadhiyo wajishushia.
Solomon ole Musere
Chuo kikuu cha Kenyatta
2011
Naketi na kutuliya, na tungo nawatungiya,
Nanena ya mausiya, mabinti waje sikiya,
Nakuomba karibiya, usije ukasusiya,
Marinda ufupishapo, hahiyo wajishushia.
Mavazi yanayoruka, sitamani kujivika,
Mapaja kubainika, sidhani utapendeka,
Maungo yakifichuka, huwezi kutamanika,
Marinda ufupishapo, hadhiyo wajishushia,
.
Marinda yanayobana, tangu lini yakafana?
Akivalia kimwana, mwenyewe ajitukana,
Wazee wakiwaona, mwajitakia laana,
Marinda ufupishapo, hahiyo wajishushia .
Mavazi yasosetiri, hakika yana ghururi,
Minofu ikithihiri, mwadhani ni umahiri?
Maungo kiwa dhahiri, laana yawasubiri,
Marinda ufupishapo, hadhiyo wajishushia.
Kivaa minisketi, tashindwa hata kuketi,
Watuonyesha magoti, mapaja kama majiti,
Maguu lau makuti, haina haiba eti,
Marinda ufupishapo, hadhiyo wajishushia.
Vazi ni fupi jamani, mwalipasua mbeleni?
Hamna haya usoni, hata kule kanisani,
Mwajivalia kihuni, hata m'wapo nyumbani,
Marinda ufushapo, hadhiyo wajishushia.
Hadi hapo mabenati, nimefikia tamati,
Mawaidha siyaati, ni ombi si sharuti,
Nawashukuru kwa dhati, kwa kunipeni wakati,
Marinda ufupisapo, hadhiyo wajishushia.
Solomon ole Musere
Chuo kikuu cha Kenyatta
2011
MAKIWA WANAKENYATTA
MAKIWA WANAKENYATTA
Bisimillahi Rabuka, illahi Mola Rahimu,
Mbelezo waja twafika, twakulilia Rahimu;
Matozi yatudondoka, twaomba uturehemu,
Makiwa wanakenyatta, kumpoteza Ogeto.
Maafa yametuzuru, mwenzetu yakatupoka,
Hakika yametudhuru, nyoyoni twasononeka,
Tumeipoteza nuru, ghafula imezimika,
Makiwa wanakenyatta, kumpoteza Ogeto.
Mswiba umetuswibu, ametuacha swahibu,
Tulimpenda ajabu, halingani na dhahabu,
Hatuna katu majibu, kwa kifo k'lichokuswibu,
Makiwa wanakenyatta, kumpoteza Ogeto.
Nakumbuka hino siku, 'lipotuacha mpasi,
Saa mbili za usiku, laili ya Jumamosi,
Huzuni ilitupiku, ukatukumba mkosi,
Makiwa wanakenyatta, kumpoteza Ogeto.
Ni pigo kwetu chuoni, kumpoteza Ogeto,
'Metuachia huzuni, na maisha ya majuto,
Tulikuenzi mwandani, kipenzi chetu Ogeto,
Makiwa wanakenyatta, kumpoteza Ogeto.
Rambi rambi nyingi sana, ziwafikie nyumbani,
Farajaze Maulana, kwa ndugu na majirani,
Inshallah tutamwona, kipenzi chetu peponi,
Makiwa wanakenyatta, kumpoteza Ogeto.
Nimefika kituoni, machozi yanikupuka,
Poleni ndugu poleni, ni matakwa ya Rabuka,
Alazwe pema peponi, apate kusalimika,
Makiwa wanakenyatta, kumpoteza Ogeto.
Solomon ole Musere
Chuo kikuu cha Kenyatta
Novemba 2011
Bisimillahi Rabuka, illahi Mola Rahimu,
Mbelezo waja twafika, twakulilia Rahimu;
Matozi yatudondoka, twaomba uturehemu,
Makiwa wanakenyatta, kumpoteza Ogeto.
Maafa yametuzuru, mwenzetu yakatupoka,
Hakika yametudhuru, nyoyoni twasononeka,
Tumeipoteza nuru, ghafula imezimika,
Makiwa wanakenyatta, kumpoteza Ogeto.
Mswiba umetuswibu, ametuacha swahibu,
Tulimpenda ajabu, halingani na dhahabu,
Hatuna katu majibu, kwa kifo k'lichokuswibu,
Makiwa wanakenyatta, kumpoteza Ogeto.
Nakumbuka hino siku, 'lipotuacha mpasi,
Saa mbili za usiku, laili ya Jumamosi,
Huzuni ilitupiku, ukatukumba mkosi,
Makiwa wanakenyatta, kumpoteza Ogeto.
Ni pigo kwetu chuoni, kumpoteza Ogeto,
'Metuachia huzuni, na maisha ya majuto,
Tulikuenzi mwandani, kipenzi chetu Ogeto,
Makiwa wanakenyatta, kumpoteza Ogeto.
Rambi rambi nyingi sana, ziwafikie nyumbani,
Farajaze Maulana, kwa ndugu na majirani,
Inshallah tutamwona, kipenzi chetu peponi,
Makiwa wanakenyatta, kumpoteza Ogeto.
Nimefika kituoni, machozi yanikupuka,
Poleni ndugu poleni, ni matakwa ya Rabuka,
Alazwe pema peponi, apate kusalimika,
Makiwa wanakenyatta, kumpoteza Ogeto.
Solomon ole Musere
Chuo kikuu cha Kenyatta
Novemba 2011
Subscribe to:
Comments (Atom)