Saturday, 21 July 2012

KONGOLE WANASIASA

Kwa moyo wa kujituma, najitolea mhanga kama mhanga kuisifia dhima sheshe wanayotekeleza wanasiasa wetu hasa hao wanaowania urais kwenye uchaguzi ujao.Nani kama wao!

KONGOLE WANASIASA
Hewaa ndugu hewaa,lau kipungu napaa,
Nangia bila fadhaa,kwa beti ziso mawaa,
Tega lako lau paa,tuwaswifu mashujaa,
Kongole wanasiasa,mafundi wa kutongoa.

Mafundi wa kutongoa,wasemi waso na doa,
Kalima mwazishopoa,kokote mnapotua,
Ahadi chekwa mwatoa, nyingine za kushitua,
Kongole wanasiasa,farisi walobobea.

Farisi walobobea,waama nawaswifia,
Kofia nawavulia,si shere nawachezea,
Kokote mwatuchochea, fulani kumchukia,
Kongole wanasiasa,walumbi wenye busara.

Walumbi wenye busara,na bonge la mishahara,
Japo nchi ni fukara,dhima yenu bar'abara,
Uchumi umedorora,'meadimika ajira,
Kongole wanasiasa,wakenya twawathamini.

Wakenya twawathamini,'tawarejesha bungeni,
'Tawatetea debeni,wangwana waso kifani,
Japo twala mapipani,pasi kivazi milini,
Kongole wanasiasa,wajumbe wasitahiki.



Wajumbe wasitahiki, nani atawadhihaki?
'Metuondelea dhiki,japo 'meinajisi haki,
Matendo yenu afiki, na ndimi tamu ja uki,
Kongole wanasiasa,maneno yenu matamu.

Maneno yenu matamu, mithili ya zamzamu,
Farisi wa kushitumu,kwa tenzi za kuhujumu,
Wajumbe nawaheshimu,japo ndimi zenu sumu,
Kongole wanasiasa,kusema kweli mwayuwa.

Kusema kweli mwayuwa,ahadi kuzipomowa,
Jukwaani mkituwa,wakata tunachachawa,
Viuno 'twavinenguwa, tuisahau shakawa!
Kongole wanasiasa, kipaji bora mnacho.

Mnacho bora kipaji,namshukuru mpaji,
Nawavisheni mataji,nimalize utungaji,
Sinione mjuaji,nguchiro mkosoaji
Kongole wanasiasa, kwa bora wenu 'wongozi.

Kikomo ninakomile,uyumbe 'meupatile,
Ziada siandikile,'nisije fumwa mishale,
Virago nafungatile,mwituni nijitomile,
Kongole wanasiasa,kwa sheshe wenu wajibu.
        SOLOMON OLE MUSERE,
        Chuo kikuu cha Kenyatta,
            NAIROBI.
            17 Julai 2012.   

No comments:

Post a Comment