Saturday, 21 July 2012

RINDA FUPI NI HALALI!

Waziri wa Elimu mheshimiwa Mutula Kilonzo amejitokeza bayana kuwaunga mkono wanafunzi waliogoma wakidai wanalazimishwa kuvaa marinda marefu zaidi....Akasema kuwa hata sketi likiwa fupi halina shida kwani watoto si "watawa!"..........Kwa muktadha huo nikalitunga shairi "kuusifu" uamuzi huu wa kipekee!

WAZIRI AMEPITISHA
Kalamu na karatasi, n'andike hili kwa kasi,
Nimimine zangu hisi,niseme zangu tetesi,
Nimpongeze farisi,nimpe kongole sisisi,
Waziri ametangaza,marinda yapande juu.

Nimependezwa hakika, ni uamuzi mwafaka,
Rinda refu ni dhihaka,kwa nchi 'loimarika,
Minofu ikifichuka,ishara "tumechanuka"
Waziri amekubali, wana wakude marinda.

Rinda hadi aridhini,halifai aswilani,
Fedheha kubwa shuleni,waziri amebaini,
Rinda refu ni la nini, kuvaliwa darasani?
Waziri amepitisha,nani wewe kuipinga?

Kidete amesimama,jukwaani akasema,
Rinda refu si salama,ni bovu tena la zama,
Fupi linalo heshima,halitazua zahama,
Waziri amepitisha,watoto wavae mini.

Binti zetu si watawa,hawafai kuonewa,
Wana uhuru kwamuwa,wapewe hino satuwa,
Tuache kuwaumbuwa,kuwashikia shokowa,
Waziri amekubali, tuvae tunavyotaka.

Kenya imeendeleya, usasa kukumbatiya,
Haifai kubakiya,nyuma mithili mikiya,
Hata mini kivaliya,wana hawana hatiya,
Mutula amepitisha,sketi refu si njema.

Mutula nakupongeza,wana 'mewatelekeza,
Wazo lako lapendeza,wizara waendeleza,
Mambo unayageuza,uzidi kutuongoza,
Waziri amepitisha, rinda fupi ni halali.

Totauti siioni,darasa na danguroni,
Kama si uhayawani, basi nambie ni nini,
Kilichobaki ni nini,Mutula tuelezeni?
Waziri amepitisha, darasa liwe danguro!

Mwisho ninahitimisha,kololo nimedondosha,
Musere ninafungasha,uyumbe 'mewasilisha,
Mutula yuatamausha,wazazi 'megadhabisha,
Waziri amepitisha,wana wavae kihuni.
        SOLOMON OLE MUSERE,
        Chuo kikuu cha Kenyatta,
            NAIROBI.
        21 Julai 2012

No comments:

Post a Comment