Bisimillahi Rabuka, illahi Mola muweza,
Mwanao nalalamika, upweke menilemaza,
Jamani nahuzunika,nani tanituliza?
Namtafuta kidosho, mwenye penzi la hakika.
Asiwe mwenye papara,ninachelea chiriku,
Kimwana wa hapa bara, mgeni nitamshuku,
Kidosho mwenye busara, asokuwa zumbukuku,
Namtafuta kidosho, mwenye penzi la hakika.
Ninamsaka tabibu, alo na mwingi mahaba,
Yangu roho aitibu, kwa mapenzi yaso haba,
Awe wa kwangu swahibu, upweke umenikaba,
Namtafuta kidosho, mwenye penzi la hakika.
Awe na bora umbile, na twabia adilifu,
Mtoto mwenye sumile,mwenye haiba faafu,
Nitalivaa penzile, shingoni lau mkufu,
Namtafuta kidosho, mwenye penzi la hakika.
Nitamtwika jukumu, yangu roho kutuliza,
Ashike hino hatamu, rohoni kuniliwaza,
Maneno yake matamu,upweke kuifukiza,
Namtafuta kidosho, mwenye penzi la hakika.
Awe na mwingi heshima, kwa wadogo na wakubwa,
Kimwana mwenye hekima, asiyetokwa ubwabwa,
Alo tayari kwa dhima, kutenda yalo makubwa,
Namtafuta kidosho, mwenye penzi la hakika.
Atanituza Rabana, tunda la roho yangu,
Matoni nikimuona, yatanitoka matungu,
Hakika tutapendana, malaika ua langu,
Namtafuta kidosho, mwenye penzi la hakika.
Kaditama wa tamati,kalamu ninailaza,
Wazo langu siliati,narudia kutangaza,
Khaherini mabenati, dhima hino mewatweza,
Namtafuta kidosho mwenye penzi la hakika.
SOLOMON OLE MUSERE
CHUO KIKUU CHA KENYATTA
2011.
No comments:
Post a Comment