Tuesday, 29 May 2012

NAMTAFUTA KIDOSHO

PENZI LA DHATI

Bisimillahi  Rabuka,  illahi   Mola  muweza,
Mwanao nalalamika, upweke menilemaza,
Jamani  nahuzunika,nani tanituliza?
Namtafuta kidosho,  mwenye penzi la hakika.

Asiwe mwenye papara,ninachelea chiriku,
Kimwana wa hapa bara, mgeni nitamshuku,
Kidosho mwenye busara, asokuwa zumbukuku,
Namtafuta kidosho, mwenye penzi la hakika.

Ninamsaka tabibu, alo na mwingi mahaba,
Yangu roho aitibu, kwa mapenzi yaso haba,
Awe wa kwangu swahibu, upweke umenikaba,
Namtafuta kidosho, mwenye penzi la hakika.

Awe  na  bora umbile, na twabia adilifu,
Mtoto mwenye sumile,mwenye haiba faafu,
Nitalivaa penzile,  shingoni  lau mkufu,
Namtafuta  kidosho, mwenye penzi la hakika.

Nitamtwika jukumu, yangu roho kutuliza,
Ashike  hino hatamu, rohoni kuniliwaza,
Maneno yake matamu,upweke kuifukiza,
Namtafuta  kidosho, mwenye penzi la hakika.

Awe na mwingi heshima,  kwa wadogo na wakubwa,
Kimwana mwenye hekima, asiyetokwa ubwabwa,
Alo tayari kwa dhima, kutenda yalo makubwa,
Namtafuta  kidosho, mwenye penzi la hakika.

Atanituza  Rabana, tunda la roho yangu,
Matoni nikimuona, yatanitoka matungu,
Hakika tutapendana, malaika ua langu,
Namtafuta kidosho, mwenye penzi la hakika.

Kaditama wa tamati,kalamu ninailaza,
Wazo langu siliati,narudia kutangaza,
Khaherini mabenati, dhima hino mewatweza,
Namtafuta kidosho mwenye penzi la hakika.

SOLOMON OLE MUSERE
CHUO KIKUU CHA KENYATTA
2011.

Friday, 11 May 2012

ULIYATAKA MWENYEWE

ULIYATAKA MWENYEWE,
Mrembo  nakuswabahi,natumai u buheri,
Fursa hino  naiwahi, kukuasa kishairi,
Nanena yalo sahihi,nikwambile  pasi siri,
Uliyataka mwenyewe, na sasa kilio chani?

Kidosho nilikupenda,posa nikakuletile,
Nawe juu ukapanda,kuwa mie mchochole,
Nenda basi mwanakwenda, Musere nikakwambile
Uliyataka mwenyewe, na sasa kilio chani?

Bwanyanye kakughilibu,ukawa windo rakhisi,
Ukalikumbatia dubu, kwa tamaa ya ukwasi,
Kirinda pasi aibu, kikakutoka kwa kasi,
Uliyataka mwenyewe, na sasa kilio chani?

Mhuni ukampa fursa, lako tunda kulimega,
Mkazamia anasa, mahaba yaliponoga,
Kila siku kawa misa, kokote mkijibwaga,
Uliyataka mwenyewe, na sasa kilio chani?

Dunia hutoiweza, nilikupa mausiya,
Matusi 'kanilekeza, kisema nakuchongeya,
Ukajigeuza pweza, makaa kujipaliya,
Uliyataka mwenyewe, na sasa kilio chani?

Hakika niliumiya,kimwana ulipozama,
Mengi nilokutendeya, ukaleta uhasama,
Kabidi kunyamaziya,kwa soni nikiinama,
Uliyataka mwenyewe, na sasa kilio chani?

Haikupita miezi, akakuponyoka Keni,
Likavuruga penzi, kitumbua mchangani,
Ukaachwa na matozi, na ndwele humo mwilini
Uliyataka mwenyewe, na sasa kilio chani?

Katu huoni fedheha, eti wajileta kwangu?
'Sitaraji msamaha, hilo muuze Mungu,
Ulotenda ni karaha,yalinitia utungu,
Uliyataka mwenyewe, na sasa kilio chani?

Kikomo ninapotia, kidosho ushasikia,
Katu sitochelea,ukweli kukuambia,
Hilo kero fikiria, ndo ujumbe nakuatia,
Uliyataka mwenyewe, na sasa kilio chani?

SOLOMON MUSERE, FEB 2012.
CHUO KIKUU CHA KENYATTA